Search This Blog

Friday, 21 October 2016

YELLOW FEVER (HOMA YA MANJANO)

Ujue ugonjwa wa Manjano.

Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi viitwavyo flavivirusUgonjwa huu huenezwa na mbu aina ya aedes aegypti na ni vigumu kuutofautisha na magonjwa mengine kama malaria kwenye dalili za mwanzo bila kutumia vipimo.

Ugonjwa huu hushambulia seli za kinga mwilini (macrophages, monocytes). 
Baada ya kuingia ndani ya seli, virusi vya homa ya manjano huzaliana na kuendelea kukua huku wakihama kutoka kwenye seli moja hadi nyingine kushambulia. Virusi huenda kwenye seli za ini na kuanza kuzishambulia na hivyo kusababisha sumu kwenye damu
DALILI ZA HOMA YA MANJANO
Baada ya kuambukizwa homa ya manjano, huchukua siku tatu hadi sita kabla ya dalili za mwanzo kuanza kujitokeza. Dalili za mwanzo za homa ya manjano ni pamoja na:
  • Homa
  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu ya mgongo
  • Kukosa hamu ya kula (anorexia)
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Uchovu na udhaifu wa mwili
Asilimia 15 ya watu wanaopata homa ya manjano huingia kwenye hatua ya pili ya ugonjwa huu, isababishwayo na kuharibika kwa ini. Hatua ya pili  inaambatana na dalili mbaya zaidi zikiwemo:
  • Jaundice (macho, ulimi na viganja kubadilika kuwa rangi ya njano)
  • Maumivu makali ya tumbo
  • Kutapika damu
  • Kutokwa na damu machoni na mdomoni (hemorrhage)
Mgonjwa akifanikiwa kupona ugonjwa huu, atakua amejijengea kinga hivyo hataweza kupata homa ya manjano maisha yake yote.

CHANJO
Chanjo ya homa ya manjano ijulikanayo kama YF-VAX® 17D inapatikana na hutotolewa kila mwaka
kwenye vituo vya afya kwa watu wote, ikiwemo wasafiri na watalii watokao nchi za nje.

MATIBABU

Matibabu ya uhakika ya homa ya manjano  hayajapatikana, kutokana na ukweli kwamba ugonjwa huu unasababishwa na virusi na hivyo hakuna dawa inayoaminika kwamba itaweza kuua kabisa virusi hivi, hivyo ni vyema kupata chanjo ya homa ya manjano kabla hujapatwa na ugonjwa wenyewe.
Wizara ya afya hutoa chanjo ya homa ya manjano kwa watoto walio chini ya miaka mitano kila mwaka hivyo ni vyema umpeleke mtoto wako siku itakapotangazwa

JINSI UGONJWA UNAVYOSAMBAZWA


Ugonjwa wa homa ya manjano huenezwa na mbu aina ya aedes, ambaye hupatikana katika maeneo ya  katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara, ikiwemo Tanzania. Mbu jike aina ya aedes hupendelea kunyonya damu pindi awapo mjamzito ili kumwezesha kurutubisha mayai yake. Mbu aliyenyonya damu ya mtu mwenye homa ya manjano huweza kumwambukiza mtu mwingine.
kitropik na savanna, ikiwemo Afrika, amerika ya kusini pamoja na mashariki ya mbali. Mbu hawa kwa Afrika hupatikana zaidi
Ugonjwa huu pia huweza kuenezwa kwa kuchangia sindano na mtu ambaye tayari ameambukizwa ugonjwa wa homa ya manjano na pia kuwekewa damu au kupandikizwa kiungo cha  mtu aliyeathirika kunaweza kusababisha maambukizi.
   

NJIA ZA KUJIKINGA NA HOMA YA MANJANO
Mbinu za kujikinga na homa ya manjano zinahusisha kujikinga kuumwa na mbu, na nyingi zinafanana na zile za kujikinga na malaria pamoja na dengue fever. Zifuatazo ni baadhi ya njia za kujikinga na homa ya manjano
:
  • Vaa nguo ndefu zinazofunika mwili vizuri
  •  Pulizia dawa ya mbu kwenye nyumba ili kuua mbu
  •  Tokomeza mazalia ya mbu kwa kufukia maji yaliyotuama, ikiwa na pamoja na makopo, vifuu pamoja na vitu vingine vinavyoweza kukinga maji.
  • Mtu akigundulika kwamba ana homa ya manjano atibiwe haraka ili kuzuia ugonjwa kusambaa
  • Usichangie sindano pamoja na watu wengine, kwani kuna hatari ya kuambukizwa magonjwa mengi ikiwemo homa ya manjano

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon

HEMATURIA (UGONJWA WA KUKOJOA DAMU)



Ugonjwa wa kukojoa damu.

Image result for kukojoa damu
HAEMATURIA ni ugonjwa wa kukojoa damu ambapo kwenye mkojo kunakuwepo chembechembe za damu nyekundu (Red blood cells).
Kukojoa damu ni dalili ya kuonyesha kuwa mtu anayekojoa ana magonjwa katika mfumo wa mkojo kama vile magonjwa ya kichocho au magonjwa mengine yanayoshambulia kibofu cha mkojo au kwenye figo.
SABABU
Magonjwa yanayoshambulia mfumo wa mkojo kama vile UTI, magonjwa ya zinaa hasa kwa wanawake, vijidudu kama staphylococcus saprophyticus, mawe kwenye figo (kidney stone) kuvimba kwa tezi zinazozalisha manii kwa wanaume ambao umri umeenda yaani wazee.
Sababu nyingine ni kama kupata ajali na kuumia sehemu za mfumo wa mkojo (trauma), kupata magonjwa kama kansa ya kibofu cha mkojo, hii hutokea mara nyingi hasa vijijini ambapo watu wanacheza au kuogelea kwenye madimbwi ya maji yasiyotembea.
Sababu zingine ni mtu kuugua magonjwa ya sickle cell anemia na magonjwa mengine ya figo kama vile nephotic syndrome na mengine mengi ambayo yanajulikana kwa kitaalamu na siyo rahisi kuyafafanua kwa Kiswahili.
AINA YA UGONJWA WA KUKOJOA DAMU
Kuna aina mbili za damu kutoka kwenye mkojo, moja ni ile ambayo damu huchuruzika na kuonekana vizuri kwenye mkojo. Hii hujulikana kama macroscopic haematuria au gross haematuria ambayo hutokea kwa wagonjwa wa kichocho au waliopata ajali.
Nyingine ni ile inayoonekana kwa mbali na mara nyingine huonekana wakati mgonjwa anapopimwa mkojo, aina hii hujulikana kama microscopic haematuria.
JINSI YA KUGUNDUA TATIZO (diagnosis)
Mara nyingi tatizo la kukojoa damu hugundulika baada ya mgonjwa kwenda hospitalini na kuonana na daktari na akachukua maelezo yake vizuri na kuagiza mgonjwa akapime mkojo.
Kipimo cha Ultrasound pia husaidia kujua tatizo linalosababisha mgonjwa akojoe damu.
Mashine ya X- ray husaidia kugundua kama mgonjwa ana mawe kwenye figo. Kipimo kingine cha kisasa ni CT scan hiki kina uhakika ila ni ghali sana na hupatikana kwenye hospitali kubwa.
TIBA
Tiba ya uhakika ni kujua sababu inayosababisha mgonjwa akojoe damu kama ni kichocho basi mgonjwa atapewa dawa ya kichocho na kama ni UTI mgonjwa atapewa dawa husika na kama ni magonjwa ya zinaa nayo yatatibiwa. Magonjwa mengine ni kama yale ya figo basi nayo yakigundulika yatatibiwa.
USHAURI
Watoto wasichezee maji yaliyosimama hasa kwenye mabwawa vijijini na mijini, wakigundulika kuwa walicheza basi haraka wapelekwe hospitali kupimwa.
KWA NINI USILE TENA MKATE
MWEUPE KUANZIA LEO?

Mkate ndiyo chakula kikuu cha kila siku cha familia nyingi duniani, hasa sehemu za mijini na ndiyo chakula kinachotumika na watu wa rika zote, wakubwa kwa wadogo, lakini ni wangapi tunajua kuwa mkate mweupe, ambao ndiyo chaguo namba moja la familia nyingi, ni hatari kwa afya zetu?
Kuna msemo maarufu wa Kiingereza kuhusu mkate mweupe usemao: The Whiter the Bread, the Quicker You are Dead! kwa tafsiri isiyo rasmi, msemo huu unamaanisha kuwa ‘kadiri unavyopenda kula mkate mweupe, ndivyo utakavyokufa haraka!’ Amini, usiamini, mkate mweupe siyo mzuri kwa afya yako!
Inawezekana kabisa habari hii isikufurahishe, lakini kama kweli unataka kuboresha afya yako, unapambana na suala la kupunguza unene, unataka kujiepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari (Type II), ugonjwa wa moyo au saratani ya tumbo, basi huna budi ya kuachana na mkate mweupe.
Kama tulivyosisitiza kila mara katika makala zetu nyingi za nyuma kuwa vyakula vyote vitokanavyo na nafaka zilizokobolewa vina hasara zaidi kiafya kuliko faida, mkate mweupe nao ni miongoni mwa vyakula hivyo.
KWA NINI USILE MKATE MWEUPE?
Kama ujuavyo, mkate unatengenezwa kutokana na ngano na mkate mweupe unatokana na unga wa ngano iliyokobolewa na kuondolewa virutubisho vyake muhimu vya asili ambavyo huwa muhimu katika uimarishaji wa mfumo wa usagaji na umeng’enyaji chakula tumboni (Digestive system and metabolism).
Ili unga uwe mweupe, ngano baada ya kukobolewa husafishwa kwa mashine maalumu kwa kutumia kemikali na joto kali, kitendo ambacho huondoa kabisa virutubisho vinavyoweza kuwemo kwenye nafaka na hivyo kuiacha punje ya ngano ikiwa nyeupe na kubaki makapi.
Makapi hayo, baadaye husagwa na kuwa unga safi na mweupe ambao hutayarishwa kabla ya kutengenezwa mkate kwa kupitia hatua mbalimbali, ikiwemo hatua ya kuwekewa hamira ili uumuke, kuongezewa sukari pamoja na chumvi ili kuongeza ladha.
MADHARA YANAYOWEZA KUKUPATA KWA KULA MKATE MWEUPE
Madhara ya kwanza unayoweza kuyapata kwa kupenda sana kula mkate mweupe ni ugonjwa wa kisukari. Utafiti unaonesha kuwa mkate au chakula chochote kilichotengenezwa kutokana na unga mweupe kina kiasi kingi cha wanga ambao husababisha kuongezeka sukari mwilini.
Madhara mengine yatokanayo na mkate mweupe ni kuongezeka kwa lehemu (bad LDL cholesterol) kwenye damu, hali ambayo inaweza kusababisha presha au magonjwa ya moyo yatokanayo na kusinyaa au kuziba kwa mishipa ya damu.
Madhara hayajaishia hapo, mengine yanayoweza kukupata ni tatizo la ukosefu wa choo kwa muda mrefu. Mkate mweupe huchangia kuvuruga mfumo wa umeng’enyaji wa chakula tumboni (metabolism). Mwili unapokuwa hauna virutubisho vya kutosha, usagaji na uondoaji wa sumu mwilini huwa wa shida na uchafu unaporundikana tumboni kwa muda mrefu bila kutoka, husababisha kansa ya tumbo!
ULE NINI BADALA YA MKATE?
Kuna aina nyingine ya mkate ambayo ndiyo unayopaswa kula, mkate huo ni BROWN BREAD au MKATE MWEUSI kama unavyojulikana na wengine. Mkate huu hutengenezwa kutokana na ngano isiyokobolewa hivyo kuwa na virutubisho vyake asilia vinavyohitajika mwilini na kuwa na faida zitakazokuepusha na kupatwa na madhara yaliyotajwa hapo juu. Mkate huu hauna sukari wala chumvi, hivyo kuwa bora zaidi kwa afya yako. Kama kweli unajijali, utaacha kula mkate mweupe na kuanza kula huu mweusi leo

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon

Thursday, 20 October 2016

ASTHMA (PUMU)



Ufahamu ugonjwa wa pumu 

Image result for asthma
Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko uvimbe sugu mwilini kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii na kuwa na ute mzito hivyo kupungua kwa njia ya kupitishia hewa.
Hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Tatizo hili linaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.
Kutokana na kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua hewa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease .
Mtu aliye na pumu huwa na kipindi ambacho hawi na tatizo la pumu mpaka pale mwili unapochokozwa na kuingia katika hali hiyo. Wakati huo hote cha maisha yake kinachotokea ni kutulia tu mpaka pale inapotekea uchokozi mwilini.
Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili, iko pumu ya ghafla ijulikanayo kitabibu kama Acute asthma. Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao za hewa isiyobadilika wakati wa shambulio na usio wa shambulio.
Kundi nyingine ni Pumu sugu (Chronic Asthma). Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu njiaza hewa huzidi kuwa nyembamba na kusinyaa zaidi.

Aina za pumu
Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni inayobadilika, isiyobadilika, ya mazoezi na inayosababishwa na kazi.
Pumu inayobadilika (brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia kwa matukio ya ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili.
Aina ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.
Aina ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma) ni pumu ambayo mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack) wakati hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.
Pumu hatari isiyobadilika (status asthmaticus): Hii ni aina ya pumu iliyo hatari zaidi kwa mgonjwa. Pamoja na matumizi ya dawa kadhaa, zikiwemo vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili (steroids), mgonjwa wa aina hii ya pumu anaweza asipate nafuu ya haraka na anaweza kupoteza maisha.
Pumu inayosababishwa na mazoezi: Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya viungo. Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia pua na kupitia mdomo.
Hata hivyo, wakati mwingine hutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani na hivyo kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa.
Hali hii husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa.
Inashauriwa sana kwa watu wenye matatizo kama haya kupasha moto misuli kwa mazoezi mepesi kabla ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu.
Pumu inayosababishwa na aina ya kazi: Mazingira ya kazi yanaweza kusababisha kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hili.
Aina hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma, unga, mbao na nguo.
Pumu husababishwa na nini?
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha kutokea kwa pumu au yanayohusishwa na shambulizi lake. Mambo hayo ni pamoja na matatizo ya vinasaba, maendeleo ya kiuchumi, magonjwa ya mapafu, moshi wa tumbaku, dawa za kushusha shinikizo la damu, uchafuzi wa mazingira, msongo wa mawazo na kichanga kuanza kutumia antibiotiki mapema.
Matatizo ya kinasaba yamehusishwa na kutokea kwa karibu asilimia 90 ya ugonjwa wa pumu hususani kipindi cha utoto.
Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.
Ugonjwa wa pumu umeonekana sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ikilinganishwa na nchi zenye maendeleo na hali duni ya kiuchumi. Sababu bado hazijawa wazi.
Magonjwa ya mapafu kama bronchitis, vyanzo vya mzio kama vile vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya vyakula, vinaweza kuchoche tatizo hilo.
Uchafuzi wa mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali, Baadhi ya kemikali kwenye maeneo ya kazi hasa kwenye viwanda kama vya rangi, chuma, sementi na vigae.
Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers kama vile propanolol wapo katika hatari ya kupata shambulio la ugonjwa wa pumu.
Magonjwa kwenye mfumo wa kupumua yasabishwayo na baadhi ya virusi na bakteria kama vile rhinovirus, Chlamydia pneumonia au Bordetella pertusis.
Matumizi ya mapema sana ya baadhi ya dawa hasa antibiotiki kwa watoto yanaweza kubadilisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kumfanya mtoto kuwa katika hatari ya kupata pumu.
Ongezeko la msongo wa mawazo huweza kusababisha pumu na matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Upasuaji wakati wa kujifungua (caesarian section), Tafiti kadhaa zimeonyesha kuwa kujifungua kwa njia ya upasuaji huongeza uwezekano wa kupata pumu kwa vile njia hiyo yaweza kuathiri mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya maradhi.
Vihatarishi vya ugonjwa wa pumu
Uwezekano wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu atakuwa na magonjwa ya mzio kama vile magonjwa ya ngozi (eczema) au homa isababishwayo na aina fulani ya vumbi, vumbi la maua au chavua, matumizi ya asprini na maambukizi ya ugonjwa wa virusi.
Vile vile kama anaishi sehemu zenye baridi au hewa yenye unyevu na vumbi, matatizo katika njia yake ya chakula ikiwamo uchokozi wa kujaa tindikali na gesi tumboni.
Dalili za ugonjwa wa pumu
Dalili za ugonjwa wa pumu ni pamoja na kuishiwa na pumzi, kupumua kwa shida huku pumzi zikikata, kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing), kukohoa sana hasa nyakati za usiku au asubuhi. Kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.
Kubana kwa kifua kwa mtu aliyepata shambulizi kubwa la pumu na atashindwa kuzungumza na pia kuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa huku.
Matibabu ya Pumu
Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi/ vianzisha mzio vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya.
Kwa wagojwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili.
Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Vilevile inashauriwa kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo huweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu.
Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants) na dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators).
Zipo dawa pia pia za kuondoa mcharuko mwili na zile za kuzuia mzio Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri.
Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa, (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya oksijeni.
Vilevile dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni kuepuka visababishi na matumizi ya dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa.
Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu. Dawa hizi huleta uchokozi na mgonjwa hupata kikohozi na kubanwa.

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon

HERNIA (NGIRI)

Namna mtu anavyopata ugonjwa wa Ngiri (Hernia)

TATIZO LA NGIRI (HERNIA)Image result for HERNIA
Ngiri au Hernia ni aina ya ugonjwa ambao unampata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini zinazoshikiria au kubeba viungo (organs) fulani mwilini kupoteza uimara wake au kuwa na uwazi (Opening) na hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiriwa ipasavyo katika sehemu vinapostahili kuwepo.
Katika mwili wa binadamu, maeneo ambayo tatizo hili hutokea mara kwa mara ni maeneo ya tumboni, katika eneo la kinena, eneo la paja kwa juu na pia ngiri inaweza kutokea katika eneo ambalo mtu alifanyiwa upasuaji (operesheni).
Tatizo la ngiri huweza kumpata mtu yeyote.

Miongoni mwa vitu vinavyoweza kumsababisha mtu apate ugonjwa wa ngiri ni: Kuwa na uzito mkubwa wa mwili au kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya kubeba au kunyanyua vitu vizito, tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa muda mrefu, ujauzito au matatizo yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa kujifungua pia kuharisha au kuvimbiwa (Constipation).


Vitu hivyo pamoja na mtu kuwa na misuli au tishu zilizopoteza uimara au uwazi (opening or hole) humfanya mtu apate ngiri (hernia).
Ngiri hutambuliwa kwa kutokea kitu kama uvimbe au kujaa katika eneo husika (baadhi ya maeneo yametajwa hapo juu) na pia kwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara na daktari huwezesha kugundua tatizo hili.
Njia inayoweza kutatua tatizo hili ni kwa mtu mwenye ngiri kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha misuli au tishu zilizolegea.

Pia kutegemeana na kihatarishi cha tatizo hili, mtu unaweza kuwa unafanya mazoezi ili kupunguza uzito wako na kuweka utaratibu mzuri wa kula chakula kinachojumuisha mboga mboga au matunda yenye nyuzi nyuzi (fibers), hii itasaidia pia mmeng’enyo (digestion) wa chakula tumboni na kuepusha kuvimbiwa.


Matunda (Vitamin C) husaidia kuunganisha tishu zilizolegea na pia husaidia kupona haraka kwa sehemu iliyofanyiwa upasuaji (operesheni).

Na kama tatizo lako ni la kukohoa kwa muda mrefu kunakosababishwa na uvutaji wa sigara, ni vyema ukasitisha uvutaji ili kupunguza madhara au makali ya ngiri lakini pia kusitisha sigara kwa ajili ya usalama wa afya yako

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon

CHOLERA (KIPINDUPINDU)

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu

Image result for CHOLERA
KATIKA toleo hili tuangalie ugonjwa wa Kipindupindu. Kipindupindu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aina Vibrio cholera.

Ugonjwa huu ni moja ya magonjwa ya nayoiathiri jamii hasa pale unapotokea kwani ni miongoni mwa magonjwa ya milipuko.

Ugonjwa huu uambukizwa kutokana na vimelea vinavyopendelea kuishi kwenye kinyesi cha binadamu.

Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa kwa kunywa maji au kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya kipindupindu.


Hata hivyo baadhi ya vimelea hufanikiwa kukwepa tindikali hiyo na kuendelea kuishi.

Vimelea hivyo vilivyofanikiwa kukwepa tindikali hiyo hujishikisha kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo kwa kutumia maumbo maalum yaliyomo kwenye mwili wa binadamu ambayo huwezesha kusafiri ambayo kwa kitaalamu huitwa flagella.

Vimelea hivyo viwapo kwenye utumbo mdogo hutoa sumu iitwayo CTX au CT(cholera toxin) ambapo sumu hiyo husababisha mtu kuhara choo chenye majimaji.

Licha ya kutoa sumu hiyo pia huendelea kutoa kizazi kingine cha vimelea hao nje kwa njia ya haja kubwa.

Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo chochote cha maji au chakula watu wengine huweza kuambukizwa kipindupindu.

Maambukizi yake
Kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio cholerae zinazosababisha kuhara majimaji yenye rangi kama maji ya mchele.

Kipindupindu hutokea hasa pale mazingira yanapokuwa sio safi kwa kiasi kikubwa kwani maji, vyakula, hata vyoo huweza kuwa katika hali ya uchafu.

Bakteria ya vibrio cholerae hupatikana hasa katika kinyesi na maji ya choo na pia katika maji ya bahari, maziwa na mito kama maji machafu huingizwa katika magimba ya maji bila kusafishwa kwanza.

Katika mazingira yenye maji ya bomba, yaliyosafishwa na karakana ya kusafisha maji machafu, kipindupindu hutokea mara chache sana.

Dalili zake
  1. Dalili za awali za kipindupindu ni pamoja na kuhara ghafla choo chenye majimaji (kinakuwa na maji kama ya maji ya mchele) na choo hicho muda mwingine huwa na harufu kali kama shombo ya samaki. 
  2. Kutapika .
  3. Pia mgonjwa huonyesha dalili za kupungukiwa na maji mwilini kama vile ngozi kuwa kavu, midomo kukauka, mgonjwa kuhisi kiu kikali, kupata mkojo kidogo sana. Pia mgonjwa huwa na homa kali.
  4. Kuishiwa nguvu na kujisikia mchovu sana pamoja na macho kutumbukia ndani hasa kwa watoto


Jinsi ya kutambua ugonjwa huu
Ugonjwa huu huweza kugunduliwa na kutambuliwa kwa kuona dalili zake.

Hata hivyo ili kudhibitisha kuwa kama dalili alizonazo mgonjwa zinatokana na ugonjwa huo vipimo vifuatavyo huweza kutumika kuwa na uhakika zaidi.

Mgonjwa huweza kupimwa damu kwa hajili ya kuotesha vimelea vya kipindupindu katika maabara.

Pia choo cha mgonjwa huweza kuchunguzwa kwa kutumia darubini(dark field microscope) ambapo kama ugonjwa ni wenyewe vimelea huweza kuonekana.

Tiba
Mgonjwa wa kipindupindu huweza kupatiwa matibabu huku lengo kuu likiwa ni kurejesha maji na madini mwilini aliyoyatoa kwa njia ya kuhara au kutapika.

Njia itumikayo kumpatia maji hayo ni kwanjia ya mdomo ambapo hupewa anywe au kwanjia ya mshipa wa damu ambayo kitaalamu hujulikana kama intravenously(i.v)

Mgonjwa hunyweshwa maji mengi, kwa sababu mwili wake hupoteza maji mengi anapougua maradhi haya kwa njia ya kuhara na kutapika.

Dawa zinazojulikana kufanya kazi ni kama
cotrimoxazole, erythromycin, doxycycline, chloramphenicol, na furazolidone.

Jinsi ya kujikinga na kipindupindu
  1. Miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kuepuka na kupatwa na ugonjwa huu ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
  2. Watu wengi wanatakiwa kuhakikisha wanapata maji safi na salama huku kabla ya kunywa maji hayo wanahakikisha wameyachemsha na kuyachuja pamoja na kuyahifadhi kwenye chombo safi.
  3. Ni muhimu kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kila mara baada ya kutoka chooni ili kuepuka kula au kushika chakula chochote huku mikono ikiwa michafu.
  4. Pia jamii inashauriwa kufunika chakula kikiwa mezani ili nzi wasiweze kutua juu yake
  5. Licha ya kuzingatia usafi pia inashauliwa kujenga choo angalau mita 30 kutoka kilipo chanzo cha maji pamoja na kuweka mazingira katika hali ya usafi kwa ujumla.
  6. Ili kuweza kuepuka ugonjwa Dk Chirwa anasema kuwa jamii inatakiwa kuzingatia usafi ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa kutumia sabuni.
  7. Hii ni muhimu sana hasa kwa watoto wanapokuwa shuleni ili kuepuka kupatwa na ugonjwa huo.
  8. Pia ni muhimu kunawa kabla ya kuandaa chakula au kula huku ukizingatia usafi wa vyombo vinavyotumika kuandalia chakula au kulia chakula hicho.
  9. Kusafisha matunda kwa maji safi na salama hasa ya uvuguvugu kabla ya kuyamenya au kuyala kwa yale yasiyohitaji kumenywa.
  10. Kufunika chakula ili kuepusha uwezekano wa wadudu hasa nzi kutua juu ya chakula hicho kwani wanaweza kuacha baktelia wanaoweza kuwa wamewabeba kwenye miguu yao.
  11. Maji ya choo yanayotokana na wagonjwa wa kipindupindu yanapasa kupitia mashimo ya choo yaliyohifadhiwa vizuri ili kuzuia usambazaji wa bakteria
  12. Vifaa vyote vinavyotumiwa na wagonjwa vinapaswa kuchemshwa kwa maji ya moto.
  13. Mikono inayoshika wagonjwa au nguo zao inapaswa kusafishwa kwa maji na sabuni.
  14. Mashimo ya choo yanapaswa kutiwa dawa za kuua bakteria kwa kutumia klorini

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon