Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu
KATIKA toleo hili tuangalie ugonjwa wa Kipindupindu. Kipindupindu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aina Vibrio cholera.
Ugonjwa huu ni moja ya magonjwa ya nayoiathiri jamii hasa pale unapotokea kwani ni miongoni mwa magonjwa ya milipuko.
Ugonjwa huu uambukizwa kutokana na vimelea vinavyopendelea kuishi kwenye kinyesi cha binadamu.
Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa kwa kunywa maji au kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye vimelea vya kipindupindu.
Hata hivyo baadhi ya vimelea hufanikiwa kukwepa tindikali hiyo na kuendelea kuishi.
Vimelea hivyo vilivyofanikiwa kukwepa tindikali hiyo hujishikisha kwenda kwenye ukuta wa utumbo mdogo kwa kutumia maumbo maalum yaliyomo kwenye mwili wa binadamu ambayo huwezesha kusafiri ambayo kwa kitaalamu huitwa flagella.
Vimelea hivyo viwapo kwenye utumbo mdogo hutoa sumu iitwayo CTX au CT(cholera toxin) ambapo sumu hiyo husababisha mtu kuhara choo chenye majimaji.
Licha ya kutoa sumu hiyo pia huendelea kutoa kizazi kingine cha vimelea hao nje kwa njia ya haja kubwa.
Iwapo choo hicho cha mtu aliyeambukizwa kipindupindu kitachanganyika na chanzo chochote cha maji au chakula watu wengine huweza kuambukizwa kipindupindu.
Maambukizi yake
Kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio cholerae zinazosababisha kuhara majimaji yenye rangi kama maji ya mchele.
Kipindupindu hutokea hasa pale mazingira yanapokuwa sio safi kwa kiasi kikubwa kwani maji, vyakula, hata vyoo huweza kuwa katika hali ya uchafu.
Bakteria ya vibrio cholerae hupatikana hasa katika kinyesi na maji ya choo na pia katika maji ya bahari, maziwa na mito kama maji machafu huingizwa katika magimba ya maji bila kusafishwa kwanza.
Katika mazingira yenye maji ya bomba, yaliyosafishwa na karakana ya kusafisha maji machafu, kipindupindu hutokea mara chache sana.
Dalili zake
- Dalili za awali za kipindupindu ni pamoja na kuhara ghafla choo chenye majimaji (kinakuwa na maji kama ya maji ya mchele) na choo hicho muda mwingine huwa na harufu kali kama shombo ya samaki.
- Kutapika .
- Pia mgonjwa huonyesha dalili za kupungukiwa na maji mwilini kama vile ngozi kuwa kavu, midomo kukauka, mgonjwa kuhisi kiu kikali, kupata mkojo kidogo sana. Pia mgonjwa huwa na homa kali.
- Kuishiwa nguvu na kujisikia mchovu sana pamoja na macho kutumbukia ndani hasa kwa watoto
Jinsi ya kutambua ugonjwa huu
Ugonjwa huu huweza kugunduliwa na kutambuliwa kwa kuona dalili zake.
Hata hivyo ili kudhibitisha kuwa kama dalili alizonazo mgonjwa zinatokana na ugonjwa huo vipimo vifuatavyo huweza kutumika kuwa na uhakika zaidi.
Mgonjwa huweza kupimwa damu kwa hajili ya kuotesha vimelea vya kipindupindu katika maabara.
Pia choo cha mgonjwa huweza kuchunguzwa kwa kutumia darubini(dark field microscope) ambapo kama ugonjwa ni wenyewe vimelea huweza kuonekana.
Tiba
Mgonjwa wa kipindupindu huweza kupatiwa matibabu huku lengo kuu likiwa ni kurejesha maji na madini mwilini aliyoyatoa kwa njia ya kuhara au kutapika.
Mgonjwa wa kipindupindu huweza kupatiwa matibabu huku lengo kuu likiwa ni kurejesha maji na madini mwilini aliyoyatoa kwa njia ya kuhara au kutapika.
Njia itumikayo kumpatia maji hayo ni kwanjia ya mdomo ambapo hupewa anywe au kwanjia ya mshipa wa damu ambayo kitaalamu hujulikana kama intravenously(i.v)
Mgonjwa hunyweshwa maji mengi, kwa sababu mwili wake hupoteza maji mengi anapougua maradhi haya kwa njia ya kuhara na kutapika.
Dawa zinazojulikana kufanya kazi ni kama cotrimoxazole, erythromycin, doxycycline, chloramphenicol, na furazolidone.
Jinsi ya kujikinga na kipindupindu
- Miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kuepuka na kupatwa na ugonjwa huu ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama.
- Watu wengi wanatakiwa kuhakikisha wanapata maji safi na salama huku kabla ya kunywa maji hayo wanahakikisha wameyachemsha na kuyachuja pamoja na kuyahifadhi kwenye chombo safi.
- Ni muhimu kunawa mikono kwa maji safi na sabuni kila mara baada ya kutoka chooni ili kuepuka kula au kushika chakula chochote huku mikono ikiwa michafu.
- Pia jamii inashauriwa kufunika chakula kikiwa mezani ili nzi wasiweze kutua juu yake
- Licha ya kuzingatia usafi pia inashauliwa kujenga choo angalau mita 30 kutoka kilipo chanzo cha maji pamoja na kuweka mazingira katika hali ya usafi kwa ujumla.
- Ili kuweza kuepuka ugonjwa Dk Chirwa anasema kuwa jamii inatakiwa kuzingatia usafi ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na salama kwa kutumia sabuni.
- Hii ni muhimu sana hasa kwa watoto wanapokuwa shuleni ili kuepuka kupatwa na ugonjwa huo.
- Pia ni muhimu kunawa kabla ya kuandaa chakula au kula huku ukizingatia usafi wa vyombo vinavyotumika kuandalia chakula au kulia chakula hicho.
- Kusafisha matunda kwa maji safi na salama hasa ya uvuguvugu kabla ya kuyamenya au kuyala kwa yale yasiyohitaji kumenywa.
- Kufunika chakula ili kuepusha uwezekano wa wadudu hasa nzi kutua juu ya chakula hicho kwani wanaweza kuacha baktelia wanaoweza kuwa wamewabeba kwenye miguu yao.
- Maji ya choo yanayotokana na wagonjwa wa kipindupindu yanapasa kupitia mashimo ya choo yaliyohifadhiwa vizuri ili kuzuia usambazaji wa bakteria
- Vifaa vyote vinavyotumiwa na wagonjwa vinapaswa kuchemshwa kwa maji ya moto.
- Mikono inayoshika wagonjwa au nguo zao inapaswa kusafishwa kwa maji na sabuni.
- Mashimo ya choo yanapaswa kutiwa dawa za kuua bakteria kwa kutumia klorini
Prepared by Dr Salim Amour
Cardio_thoracic Surgeon
No comments:
Post a Comment