Kukabili fangasi kwenye vidole vya miguu.
Tunapozungumzia maradhi ya fangasi wengi wetu hatujisikii vizuri kabisa yaani kwa kifupi hili somo si kipenzi cha wengi wetu. Hii inatokana na jinsi maradhi haya yanavyojionyesha. Mara nyingi hutokea kwenye sehemu ambazo ni aibu kuzizungumzia au kuzionyesha.
Bahati nzuri ni kuwa wala hatutakiwi tuone aibu kuzungumzia magonjwa haya kwani wengi wetu wanapata maradhi haya na yanahitaji matibabu.
Inasemekana Mtanzania mmoja kati ya watano hupata maradhi ya fangasi zaidi ya mara moja katika kipindi cha maisha yao.
Ingawa wengi wetu tunaona vibaya kuongelea maradhi yaletwayo na fangasi, viumbe hivi vinafurahisha sana ukivisoma na kuvifahamu.
Zamani sana kabla sayansi haijaendelea sana wanasayansi walidhani fangasi ni mimea lakini baada ya maendeleo ya vifaa vya uchunguzi, walitolewa kwenye kundi la mimea.
Leo ninazungumzia kuhusu tatizo la fangasi wa vidole vya miguuni ni tatizo sugu kutokana na kuwakumba wengi hapa nchini na kuwasababishia usumbufu mkubwa.
Aina hii ya fangasi hushambulia vidole vya miguu peke yake na mara nyingi hushambuli maeneo ya katikati ya vidole vya miguu hasa kati ya kidole cha tatu na nne na kile kidogo, tunachokihesabu ni cha tano.
Fangasi hawa husababisha eneo la ngozi lililoshambuliwa kuwasha, ngozi kutoka na kubadilika kwa rangi ya ngozi na kuwa nyeupe.
Mara nyingine huweza kusababisha malengelenge kutokea pia.
Fangasi za miguu hushambulia ngozi iliyo na majimaji hivyo ni rahisi zaidi kupata mashambulizi kama ngozi ya miguu inakosa ukavu.
Mifano michache ya mambo ambayo husababisha ngozi isikauke ni kama vile kuvaa viatu vya kufunika muda mrefu na kuruhusu jasho kutoka kwenye miguu bila miguu hiyo kukauka.
Namna nyingine ni kuvaa viatu vya kufunika mara tu baada ya kujimwagia miguu maji bila ya kuikausha.
Wengine ni watu wenye tatizo la kutoka jasho kwa wingi mwilini, kufanya kazi katika mazingira yanayolazimisha miguu kuwa kwenye maji kwa muda mrefu na wanaooga kwenye bafu zinazotumiwa na watu wengi kama vile shule za bweni na kambi.
Tatizo jingine ni la wale wanaotembea pekupeku kwenye ardhi iliyoloana au yenye maji kwa muda mrefu na wale wanaoshirikiana kuvaa viatu au soksi.
Haya ni makundi machache ya wale wanaoweza kupata maambukizi ya maradhi haya. Kuna wengine ambao hatuwezi kuwaweka kwenye kundi na hii inatokana na ukweli kuwa maradhi haya huweza kuambukizwa kirahisi sana. Mara nyingi maradhi haya hutambulika kwa macho tu.
Kwa kutazama eneo ambapo maradhi haya yameshambulia na mwonekano wa ngozi unaweza kutambua ni tatizo la fangasi.
Matibabu ya maradhi haya ni rahisi sana. Kinachohitajika ni ukavu wa eneo husika na baada ya hapo ni uwekaji wa dawa ambazo zinapatikana kwa wingi kwenye maduka ya dawa.
Prepared by Dr Salim Amour
Cardio_thoracic Surgeon
No comments:
Post a Comment