Search This Blog

Thursday, 13 October 2016

UGONJWA WA KIFAFA

Ufahamu kiundani ugonjwa wa Kifafa.

Ugonjwa wa kifafa ni nini?
Huu ni ugonjwa amabao unasabababishwa na seli za mishipa ya fahamu zilizopo kwenye ubongo  kutoa umeme[impulses] mwingi kuliko kawaida kwenda kwenye misuli na sehemu zingine za mwili, na matokeo yake mtu huanza kupata degedege ya mwili mzima, kukakamaa, kuanguka chini na kupoteza fahamu..
mwaka 2013 ugonjwa huu uliua zaidi ya watu laki moja duniani, 80% wakiwa waafrika.
Mgonjwa huyu huweza kuanguka mara kadhaa kwa mwezi lakini anaweza asianguke kabisa kama anafuata masharti na utaratibu mzuri wa matibabu
Chanzo cha ugonjwa huu ni nini?
chanzo kikuu cha ugonjwa huukwa watu wengi hua hakifahamiki lakini baadhi ni moja ya sababu za kuugia kifafa.
Kurithi; familia na koo zingine zinakua na ugonjwa huu hivyo watoto na wajukuu huzaliwa tayari na ugonjwa huu.
Kuumia kichwa: ajali zinazohusisha kuumia kwa kichwa huweza kusababisha kuumia kwa mishipa ya fahamu na mtu kuugua kifafa.
Ulaji wa nyama ya nguruwe; nyama ya nguruwe ina mnyoo kitaalamu unaitwa taenia solium ambao hushambulia mishipa ya fahamu ya ubongo na kumfanya mtu kuugua kifafa hivyo ni vizuri ipikwe kwa muda mrefu ili iive kabisa.
Magonjwa mengine; kuna magonjwa mtu akiugua maishani mwake baadae huweza kupata kifafa kwasababu magonjwa hayo yanavyoharibu mfumo wa ubongo.. mfano homa ya uti wa mgongo kitaalamu kama meningitis.
Uvimbe kwenye ubongo: matatizo ya uvimbe kwenye ubongo kama kansa huweza kusababisha mtu kuugua kifafa.
Kiharusi; huu ni ugonjwa ambao husababishwa na damu kushindwa kupita vizuri kwenye ubongo au kupasuka kwa mishipa ya damu ya ubongo hali hii husababisha mtu kupooza nusu ya mwili wake na huweza kuugua kifafa baadae.
Matatizo wakati wa kuzaliwa: wakati mwingine mototo huzaliwa kwa shida sana kwa njia ya kawaida kiasi kwamba kichwa chake hubanwa sana wakati wa kupita na  hali hii huweza kumsababishia kifafa kwanzia utotoni.
Matatizo ya utengenezaji wa mtoto tumboni; wakati mwingine ile miezi mitatu ya kwanza ambayo mtoto ndio anapata viungo tumboni huweza kutokea kasoro kwenye mfumo wa fahamu za kwenye ubongo na kumfanya apate kifafa akizaliwa.
Magonjwa ya uzee yanayoathiri ubongo; kuna magonjwa huharibu ubongo wakati wa uzee na magonjwa haya huweza kusababisha kifafa kipindi hicho.
Kuna aina mbili za kifafa…
Grand ma seizures
Hii ni aina ya kifafa ambayo inanawatokea watu wengi sana, mtu huanza kwa kuchanganyikiwa, huanguka na kupoteza  fahamu wakati mwingine kutoa povu mdomoni, hii huendelea kwa dakika kadhaa mpaka saa nzima.
Petit ma seizures
Hii ni aina ya kifafa ambayo mtu anaacha kuongea ghafla, mawazo yanatoka pale alipo kisha anaacha kuongea na baadae anarudi katika hali yake ya kawaida kama hakuna kilichotokea hapo katikati na aina hii hutokea kwa sekunde chache tu.

Vipimo vinavyofanyika kugundua kifafa…
Ugonjwa huu unaweza kutambulika kwa dalili tu lakini mara nyingi mgonjwa hupimwa vipimo tofauti ili kuweza kujua chanzo cha ugonjwa… mfano
  • Uwezo wa kufanya kazi  figo
  • Uwezo wa kufanya kazi maini
  • Kupima maji ya uti wa mgongo
  • Kupima Kaswende
  • X ray ya kifua
  • Picha ya ubongo mfano CT SCAN..

Matibabu
Kama kawaida chanzo cha ugonjwa kikipatikana mgonjwa huanzishiwa matibabu lakini kama mgonjwa alikua tayari ameshapata madhara kwenye ubongo kulingana na chanzo husika ataendelea kua na kifafa.
Ugonjwa wa kifafa hauponi kabisa, USIMALIZE FEDHA ZAKO KWA WAGANGA WA KIENYEJI naomba nisisitize hili, ukishaambiwa una kifafa au mgonjwa wako ana kifafa fuata utaratibu wa matibabu yaani kumeza dawa siku zote za maisha yako na kufuata baadhi ya masharti na utaishi maisha ya kawaida kabisa.
Matibabu yasiyo ya dawa wakati mgonjwa amekamatwa na kifafa:{non pharmacological treatment}
  • Mzuie mgonjwa asijiumize kwa kuweka kitu laini chini ya kichwa chake, ondoa vitu vikali karibu yake kama kisu, sindano au vyuma.
  • Usilazimishe kitu chochote kwenye mdomo wa mgonjwa.
  • Usimshike kuzuia mizunguko yake
  • Weka kichwa alale anaangalia upande mmoja ili  kutoa mate mdomoni.
  • Kaa na mgonjwa mpaka degedege ziishe
  • Usiweke chochote mdomoni kwa mgonjwa kama dawa au chakula mpaka apate fahamu zake.
Mtu mwenye kifafa hali hii ya kukamatwa na degedege za kifafa sio ya ajabu sana ila ukiona dalili hizi mkimbize hospitali..
  • Degedege za kifafa zaidi ya dakika kumi
  • Kutapika sana
  • Kushindwa kuona vizuri
  • Kupoteza fahamu
  • Kichwa kuuma sana.
Matibabu ya dawa..
Mgonjwa akishagundulika na kifafa ataanzishiwa dawa kama carbamizapine, phenorbabitone au zingine za kifafa na atakua anameza kila siku ili kuzuia hali hiyo ya kuanguka na kuoteza fahamu na akifuata masharti ataishi maisha ya kawaida kabisa.

Mambo yanayofanya kupata degedege za kifafa mara kwa mara..
  • Kukosa usingizi kwa muda mrefu
  • Mianga na miale ya disco
  • Unywaji wa pombe
  • Kuishiwa sukari mwilini wakati wa akisikia njaa kali.
  • Kutomeza dawa kama ilivyoelekezwa.
MWISHO; katika matibabu ya kifafa njia zote yaani za dawa na zisizo za dawa hutakiwa kutumika, kutofuata masharti  na kutomeza dawa huleta matatizo makubwa ya kiafya hata kupelekea kifo. Pia ni vizuri kutoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa husika kwa majirani au watu unaoishi nao waweze kukusaidia unaposhikwa na hali hii. watu wengi hufa kwa ugonjwa huu kwa kudhani wamerogwa au kuacha dawa baada ya kuombewa kwa imani za kidini  na kudhani wamepona hivyo jamii ni vizuri ikachukua tahadhari kwani ugonjwa huu ni hatari sana ila ni wa kawaida sana masharti yake yakifuata.

Prepared by Dr Salim Amour
    Cardio_thoracic Surgeon

No comments:

Post a Comment