Search This Blog

Friday, 21 October 2016

Unene kupita kiasi unachochea kisukari, saratani, kiharusi

Katika baadhi ya tamaduni hasa katika nchi za Afrika, unene unatajwa kuwa ni sifa, ufahari au pengine kipimo cha maisha mazuri. Aghalabu mtu anaponenepa huambiwa hongera au watu humzungumzia kuwa ana maisha mazuri.
Hata hivyo, kiafya ongezeko kubwa la kilo katika mwili wako ni hatua zinazoweza kukusogeza katika mauti.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linafafanua kitaalamu kuwa, unene kupita kiasi ni ongezeko la mafuta lisilo la kawaida mwilini linaloweza kuathiri afya.
Takwimu za kidunia kutoka WHO zinaeleza kuwa asilimia 13 ya watu walikuwa na unene kupita kiasi mwaka 2014.
Kati yao asilimia 11 walikuwa wanaume na asilimia 15 walikuwa wanawake. Takwimu za WHO zinasema zaidi kuwa kumekuwa na ongezeko mara mbili ya watu wenye unene kupita kiasi kuanzia mwaka 1980.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya binadamu, afya ya familia na vijana, Ali Mzige anasema unene kupita kiasi au kiriba tumbo ni janga la kitaifa na kiashiria cha maradhi yanayoweza kusababisha kifo.
“Katika nchi zinazoendelea unene unasababishwa na mfumo wa maisha, kwa mfano ulaji wa vyakula kama mayai, chipsi vyakula vya kusindikiwa vinasababisha unene huo,” anasema Dk Mzige.
Anasema kuwa unene kupita kiasi ni tatizo kubwa hapa nchini na lisipofanyiwa kazi linaweza kuigharimu nchi kama linavyozigharimu nchi za Magharibi kwa mfano Uingereza.
Kwa mfano Uingereza inatumia Trilioni 1.03 kwa ajili ya kupunguza unene na zaidi ya Dola 150 bilioni kupunguza unene kwa watoto.
“Watoto wanakunywa soda na juisi za kusindikwa, watu hawafanyi mazoezi na hawali mbogamboga na matunda. Ni lazima watapata kiriba tumbo,” anasema.
Anasema kuwa kutokana na unene kupita kiasi, hivi sasa hapa nchini asilimia tisa ya watu wana kisukari, wakati asilimia 25 wana shinikizo la damu. Kadhalika anasema unene unasababisha asilimia 35 ya saratani za aina zote.
“Licha ya hilo, watu milioni 2.7 wanapata saratani kwa kutokula mboga za majani na matunda na kwa kunywa pombe kupita kiasi,” anasema.
Anazungumzia zaidi adha ya unene na kusema kuwa ugonjwa wa saratani unawalenga watu wenye miaka kati ya 30 na 69, lakini hasa kama hawafanyi mazoezi na wanakula vyakula vya mafuta.
Unene sahihi ni upi?
Dk Mzige anasema unene kupita kiasi unabainika pale ambapo mtu ana uwiano usio sahihi wa urefu na unene. Kwa mfano kama mwanamke ambaye hajapata mtoto mwenye urefu wa sentimeta 164 anatakiwa awe na kilo 58. Kwa mwanaume mwenye urefu wa inchi 5 hadi 10 anatakiwa awe na Kilo 68.
“Unene ni janga la kimataifa si kwa hapa nchini, bali hata katika nchi nyingine. Katika baadhi ya nchi hasa jeshini, ukiongezeka uzito hupewi promosheni,” anasema.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa Hospitali ya Muhimbili, Innocent Mosha anasema unene pekee si chanzo cha saratani lakini unene uliozidi husababisha kuzalishwa kwa wingi kwa homoni za oestrogen ambazo husababisha saratani.
“Unene kupita kiasi husababisha kuzalishwa kwa tezi ya androgen, tezi hii hutengeneza kitu kinachoitwa aromatase ambayo husababisha kutengenezwa kwa oestrogen ambayo husababisha saratani,” anasema.
Dk Mosha anasema kila mtu ana seli za saratani lakini mwili wenyewe una mfumo wa kupambana na saratani, endapo mfumo huo utafeli basi saratani huanza kushambulia vimeng’enyo vya aromatase ambavyo hupatikana katika tishu za mwili, ubongo, nyumba ya uzazi, ngozi, mifupa na kimeng’enya hiki ni muhimu katika tendo la ndoa.
Utafiti uliofanywa na Muhihi A. J na wenzake jijini Dar es Salaam mwaka 2013 ulibaini kuwa asilimia 13 ya wanaume wana unene kupita kiasi wakati asilimia 36 ya wanawake walikuwa na tatizo hilo pia.
Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa licha ya Watanzania kuonekana kuwa na unene kupita kiasi, ni asilimia mbili tu ya wanawake walikubali kuwa wana tatizo hilo wakati kwa upande wa wanaume hakuna aliyekubali kuwa na tatizo. Hata hivyo, asilimia 87 ya kundi hilo walikubali kupunguza uzito.
Unene kwa watoto
Dk Mzige anazungumzia suala la unene kwa watoto na kusema kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la unene kwa watoto hali inayotishia usalama wa afya zao.
Anasema wazazi wengi hudhani kuwa mtoto mnene ni afya nzuri jambo ambalo anasema ni kinyume chake kwani hicho ni kiashiria cha magonjwa.
“Wazazi wanatakiwa kuelimishwa kuhusu hali hii. Unene si afya njema. Haiwezekani mtoto wa miaka mitano akawa na kilo zaidi ya 20. Hii ni hatari kwa afya yake,” anasema.
Mariam Kishumba, mkazi wa Tandika, Maguruwe anasema akiwa ni mwenye umri wa miaka 35 ana kilo 110 jambo ambalo limemsababishia kupata kisukari.
“Pamoja na kisukari lakini pia nina matatizo ya miguu, nashindwa kupumua vizuri na wakati mwingine mapigo ya moyo yanakwenda kasi,” anasema.
Chanzo cha unene kupita kiasi
Kichocheo cha unene kupita kiasi ni kula vyakula vya wanga vyenye mafuta kupita kiasi. Kukosa mazoezi ya kawaida ya viungo.
WHO inaeleza kuwa kubadilika kwa mfumo wa maisha kama kutembea kwa gari, kula vyakula vya kusindikiwa ndicho chanzo cha unene. Magonjwa mengine yanayoweza kusababishwa na unene kupita kiasi ni pamoja na maradhi ya moyo, kiharusi, magonjwa ambayo yaliongoza kwa kuua mwaka 2012.
Source: Mwananchi

Prepared by Dr Salim Amour 
Cardio_thoracic Surgeon

No comments:

Post a Comment