Search This Blog

Tuesday, 18 October 2016

UGONJWA WA KISUKARI (DIABETES MELITTUS)

Image result for diabetes mellitus


Ugonjwa wa kisukari kitaalam huitwa Diabetes Mellitus unasumbua watu wengi duniani na hutokea pale tezi kongosho au Pancrease inaposhindwa kutengeneza homoni au kichocheo aina ya Insulin.
Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa yasiyoambukiza, wengine hupata ugonjwa huo pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho cha Insulin na kusababisha kuongezeka kiwango cha sukari kwenye damu au kitaalam Hyperglycemia.
Insulin ni kichocheo au homoni inayotengenezwa na kongosho ili kudhibiti sukari katika damu mwilini.
Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa na mtu kuwa na kiwango kidogo cha Insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili.
Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwavunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu.
Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari inayoitwa Glucose ambayo ni chanzo cha nguvu mwilini huingia katika damu.
Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho au kwa kimombo Pancrease kutengeneza kichocheo cha Insulin.
Kazi ya Insulin ni kuondoa Glucose katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumiwa kama nishati.
Watu wenye ugonjwa wa kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu.
Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo. Huenda kongosho zao haziwezi kutengeneza Insulin ya kutosha au seli za mwili wao haziathiriwi na Insulin kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili.
kisukari
Kama wewe ni mnene kupita kiasi, hufanyi mazoezi kwa ukawaida au una watu wa ukoo walio na kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha sukari kwenye damu. Ongezeko la sukari kwenye damu mbali na kuwa kisababishi cha kisukari, hali hiyo inahusianishwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa akili uitwao 'DEMENTIA'.
Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa wa kisukari. Lakini lazima tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito wa kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti. Ugonjwa wa kisukari umeitwa kwa kufaa "ugonjwa unaoathiri kiini cha nishati ya mwili". Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha kifo.
Ugonjwa wa Kisukari kitaalamu hujulikana kama 'DIABETES MELLITUS'. Jina 'Diabetes Mellitus' linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha 'kunyonya' na neno la Kilatini linalomaanisha 'tamu kama asali'. Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.
NI NANI ANAWEZA KUWA NA UGONJWA WA KISUKARI?
Watu walio katika makundi yafuatayo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kisukari:-
– Wenye uzito uliozidi,
– Wenye historia ya kuwa na wagonjwa wa kisukari katika familia zao,
– Wanawake waliozaa watoto wenye kilo 4 au zaidi,
– Watu wasiojishughirisha au wasiofanya mazoezi,
– Wenye shinikizo la damu,
– Wenye msongo wa mawazo na
– Wenye matumizi makubwa ya pombe na sigara.
Watu hawa wanashauriwa kupima sukari yao kila mwaka wakiwa na umri wa miaka 45 na kuendelea.
Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi katika tumbo na kiuno chake kuliko katika mapaja yake. Mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu.
Wavutaji wa sigara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani zoea hilo hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu. Kitabu kimoja kinasema kwamba asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.
DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI
~ Kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati.
~ Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani.
~ Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati.
~ Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri.
~ Kusikia njaa kila wakati na kula sana.
~ Wanawake kuwashwa ukeni.
~ Kutoona vizuri.
~ Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake.
~ Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole.
~ Miguu kuoza na hata kupata gangrini.
~ Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu.
~ Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka.
~ Majipu mwilini.
Wenye dalili hizi wanashauriwa kupima sukari ili kubaini kama wana kisukari.
MATIBABU:
Mpaka sasa hakuna dawa ya kuondoa moja kwa moja Kisukari ingawa hasa kwa aina ya 2 watu baada ya kurekebisha vyakula wanaweza kujiweka katika hali ambayo mwili unaweza kutumia insulini yake kidogo bila ya kula vidonge au sindano. Kwa sasa, insulini haiwezi kumezwa kama dawa za kawaida, kwani protini hiyo humeng’enywa kabla haijafika kwenye damu. Dawa za kisukari za kutia ndani ni zile ambazo huchochea kongosho kutokeza insulini zaidi, nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine hudhibiti ongezeko la sukari katika damu na nyingine huwezesha chembe za mwili kupokea insulini. Kuna utafiti wa kupandikiza (transplant) ili kuongeza insulini mwilini kwa kutumia sehemu ya kongosho (pancreases) ya mtu mwingine lakini bado haujafanikiwa kuweza kutumika kama matibabu.
Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo uliofanywa na taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba ya nchini Japan, ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la (EMBO Molecular Medicine) inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huhitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulini.
LISHE KWA MTU MWENYE KISUKARI:
Baadhi ya nyakati mtu anaweza kufikwa na maafa kama misiba, matatizo ya kifamilia n.k hivyo mtu hupendelea kujiliwaza kwa kula zaidi au kupoteza hamu ya kula kabisa. Hali hizi zina athiri ugonjwa wa kisukari hivyo mtu inambidi aendelee na kula kama ilivyopendekezwa ingawa mara nyingine inaweza kuwa vigumu. Ni bora kuendelea kula milo midogo midogo ya mara kwa mara hii inasaidia kupunguza uzito wa mtu vile vile na kuifanya insulini kufanya kazi kwa kasi au ubora zaidi. Inawezekana kuwa huna njaa nyakati za kula, lakini inafaa utambue kwamba ni vyema ukila vitu vidogo vidogo vikavu kama ngano nzima na ule pamoja na tunda moja. Ulaji huu utakufanya usiwe na njaa kali wakati wa milo mikuu na kwa hivyo utakula kidogo zaidi.
Matunda ni chakula bora, lakini mengi yao yana sukari nyingi kwa hiyo ni vizuri kula si zaidi ya mawili-matatu kwa siku ukihakikisha kupunguza ulaji wa zabibu, embe, ndizi mbivu, matunda makavu kama tende, zabibu kavu, zeituni kwa vile matunda haya yana sukari nyingi. Mboga mboga ni vyakula bora na haziongezi sukari katika damu. Mboga mboga hizo hujumuisha  mabilinganya, bamia, vitunguu, kabeji, karoti, nyanya, tango, kisamvu n.k. Pia vyakula vyenye mizizi huteremsha sukari katika damu mfano njegere, kunde, mbaazi, maharage, njugu mawe, muhogo, ndizi mbichi, magimbi, viazi vikuu n.k
Epuka vyakula vya utamu-utamu kama vile halua, jelebi, laddu-laddu, peremende-pipi, asali, matunda ya kuchemsha, jamu, keki, kashata n.k na ujizoeshe kula vyakula visivyo vitamu tamu. Inafaa mtu anywe vinywaji vilivyo punguzwa utamu au kutiwa utamu wa vidonge yaani vinywaji bila sukari. Hakikisha kwa kusoma vinavyounda kinywaji unachokunywa. Vidonge vya utamu haviathiri kiwango cha sukari katika damu kwa hivyo mtu anaweza kutumia vidonge hivi kwa kutayarishia vyakula badala ya kutumia sukari ya kawaida. Vidonge hivi viko vya aina tofauti kwa mfano saccharin (sakkarin), cyclamate, acesulframe, aspartame (nutra-sweet) n.k
Punguza Maziwa yana sukari ya maziwa (lactose) kwa hivyo mtu anahitajiwa asinywe zaidi ya nusu lita kwa siku, hii ina maana maziwa aina mbalimbali kama mtindi na yoghurt bila ya matunda. Ukila jibini hakikisha shahamu iwe ya kiasi cha 18% ambayo ni sawa na gramu 18 kwa kila gramu 100 za jibini. Samaki ni wenye manufaa makuu kisiha na aina zote zinaruhusiwa. Usile mayai zaidi ya 2-3 kwa wiki.
Iwapo mtu atapatwa na magonjwa mengine juu ya ugonjwa wake wa kisukari, anatakiwa aendelee na matibabu yake ya kisukari kama kawaida. Na anategemewa apime sukari katika damu mara kwa mara zaidi kuliko kawaida kwa vile magonjwa mengine yanaweza kuifanya sukari ikapanda zaidi ingawa matibabu yanaendelea kwa ukawaida.
Wataalamu wa tiba hupendekeza kwamba watu wanaougua kisukari wabebe kitambulisho na kuvaa mkufu unaoweza kuwatambulisha. Kitambulisho hicho kinaweza kuokoa uhai hali ya dharura ikitokea kwa mfano mtu aliyepungukiwa sukari mwilini anaweza kueleweka kimakosa kuwa ana ugonjwa mwingine au kwamba yeye ni mlevi. Pia mtu anapokuwa safarini anashauriwa kukumbuka kuchukua dawa zake na kupima sukari yake pale inapobidi.
Mtu anaweza kujiuliza itakuaje nikipata mialiko ya sherehe zenye vyakula vingi ambavyo havipendekezwi kwa wagonjwa wa Kisukari? Ikiwa mtu anafuata mapendekezo ya hapo juu, anaweza mara 1-2 kwa mwezi kula mapocho pocho kama vile kwenye shughuli, mialiko, sherehe yenye vyakula vyenye mafuta, siagi na sukari kwa wingi.
JINSI YA KUEPUKA KUPATWA NA UGONJWA WA KISUKARI:
Kuna aina kuu mbili za Kisukari. Aina ya kwanza huanza hasa utotoni na kufikia sasa madaktari hawajui jinsi ya kuizuia. Ingawa zamani aina ya pili ya Kisukari ilihusianishwa tu na watu wazima, hivi karibuni imewaathiri pia watoto. Sehemu hii inazungumzia aina ya pili ambayo imeathiri asilimia 90 ya watu walio na kisukari.
~Pima kiwango cha sukari kwenye damu ikiwa una uwezekano mkubwa wa kupata kisukari.
~Kula vyakula vyenye lishe.
Punguza kiasi cha chakula unachokula. Badala ya kunywa vibywaji vyenye sukari nyingi au vinywaji vyenye kaboni kama vile soda, kunywa maji, chai au kahawa. Kula vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa badala ya vyakula vilivyochujwa sana viwandani. Kula nyama isiyo na mafuta mengi, samaki, njugu, karanga na maharage.
~Fanya mazoezi.
Kufanya mazoezi kunaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kukusaidia uwe na uzito unaofaa. Kwa kupata lishe bora na kufanya mazoezi ya kutosha watu wengine wanaougua ugonjwa wa kisukari wa Aina ya 2 wameacha kutumia Insulin angalau kwa muda fulani.
Uchunguzi mkubwa uliofanywa kuhusu wanawake ulionyesha kwamba kufanya mazoezi kidogo tu huongeza uwezo wa chembe za mwili wa kufyonza glukosi kwa msaada wa Insulin kwa zaidi ya saa 24. Hivyo, ripoti hiyo inakata kauli hii: “Kutembea na kufanya mazoezi mengi hupunguza uwezekano wa wanaeake kupata ugonjwa wa kisukari wa aina ya 2.” Wachunguzi hao wamependekeza watu wafanye mazoezi ya kiasi kwa angalau dakika 30 na ikiwezekana kila siku.
~Kupunguza unywaji wa pombe wa kupita kiasi.
~Kutotumia sigara au aina yoyote ya tumbaku.
~Kujikinga na mfadhaiko kwa kuepuka msongo wa mawazo.
Mfadhaiko huongeza sana kiwango cha sukari katika damu.
ATHARI ZA UGONJWA WA KISUKARI:
Watu wanaougua kisukari hawafi moja kwa moja kutokana na ugonjwa huo, bali hufa kutokana na magonjwa mengine kama ifuatavyo:-
~Matatizo ya moyo:
Magonjwa ya moyo huwa mara mbili zaidi ya watu walio na kisukari.
~Shinikizo la damu la juu kupita kiasi na kiharusi/kupooza(Stroke).
~Kuharibika mishipa ya damu na mishipa ya fahamu (Nerve Damage/Diabetes Neuropathy):
Hali hii husababisha ganzi inayopunguza hisia kwenye miguu na kupelekea kutohisi maumivu haswa miguuni (Diabetic foot) mfano unaweza vaa viatu vya kubana lakini usihisi hivo hata kupelekea vidonda na hata gangrini ya miguu. Kisukari ni sababu moja kubwa ya watu kukatwa miguu.
~Kuharibika figo(Diabetes Nephropathy):
Duniani kote kisukari ndio sababu kubwa ya figo kushindwa kufanya kazi(Kidney Failure).
~Kuharibika macho (Eye damage/Diabetes Retinopathy):
Sukari inaharibu mishipa ya damu iliyopo kwenye macho na kupelekea matatizo kwenye kuona na ukipofu. Duniani kote kisukari ndio sababu kubwa ya upofu kwa watu wazima.
~Kupungua nguvu za kupambana na maambukizo:
Maambukizo ya fizi, ngozi, njia ya mkojo na ukeni na kifua kikuu huwa zaidi ya mara mbili kuliko watu wasio na kisukari.
~Kupungua nguvu za kufanya kazi.
~Kupungua nguvu za kiume(Electile Dysfunction) na hivyo kuharibu mahusiano ya ndani:
Inasababishwa na kutokuwa na msukumo wa damu wa kutosha kwenye uume kwa sababu mishipa ya damu hupungua upana/ukubwa kutokana na kugandana kwa sukari(Calcification). Karibu robo ya wanaume wote huwa na tatizo hili wakishindwa kudhibiti kisukari.
~Kuathiri uchumi kutokana na matibabu ya muda mrefu:
Tiba ya kisukari ni ya maisha. Mahitaji ya dawa peke yake hayapungui shilingi za Tanzania laki nne kwa mwaka kwa mgonjwa anayehitaji insulini.
Ikiwa unayo historia katika familia sio lazima kwamba utapata ugonjwa huu. Lakini kwa wale ambao wanaweza kuupata wanaweza kuuchelewesha kwa kujitahidi kuishi maisha ya afya nzuri kwa kula vyakula bora hasa mboga mboga kwa wingi, mazoezi na kujiepusha na uzito mkubwa wa mwili. Pia kupima damu baada ya kila mwaka ikiwa una historia katika ukoo au una wasiwasi kutokana na dalili za kisukari
Prepared by 
     DR Salim Amour
Cardio-thoracic suergeon

No comments:

Post a Comment