Search This Blog

Friday 16 October 2020

𝐊𝐖𝐀𝐍𝐈𝐍𝐈 𝐔𝐓𝐈 (𝐔𝐫𝐢𝐧𝐚𝐫𝐲 𝐓𝐫𝐚𝐜𝐭 𝐈𝐧𝐟𝐞𝐜𝐭𝐢𝐨𝐧) 𝐇𝐔𝐖𝐀𝐏𝐀𝐓𝐀 𝐙𝐀𝐈𝐃𝐈 𝐖𝐀𝐉𝐀𝐖𝐀𝐙𝐈𝐓𝐎 ?

Kwa upande mwingine ujauzito ni kipindi kizuri sana kwa mwanamke yeyote yule , nina maana kwamba hakuna mwanamke anayetarajia kupata mtoto na asifurahie kuwa mjamzito , maana ujauzito ni njia ya kupata mtoto . Ila sasa pamoja na hayo yote kuna changamoto zake

Tukumbuke mwanamke anapokua mjamzito hata kinga yake ya mwili inakua chini , kwahiyo anakua rahisi sana kupata maambukizi mbalimbali

Utafiti unasema kwamba kama 8% hivi ya wajawazito wote hupata UTI inayoathiri figo, ureters na hata kibofu cha mkojo

TUANZIE HAPA , UTI NI NINI ?

Kiufupi elewa kwamba UTI ni maambukizi ya bacteria katika mfumo wa mkojo. Imegawanyika katika makundi mawili , UTI ya juu ( inahusisha Maambukizi kwenye Figo na Ureters - mirija inayotoa mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu) , na kuna UTI ya chini ( inahusisha kibofu cha mkojo na Urethra - mrija unaotoa mkojo nje ya kibofu)

Wanawame wanapata ITI kirahisi kutokana na maumbile yao (Anatomy) , kwamba uke na tundu la kutolea mkojo vipo karibu na tundu la haja kubwa , kwahiyo ni rahisi sana kwa bacteria kufika eneo la tukio 

Kati ya wiki ya 6 hadi wiki ya 24 ya ujauzito ndicho kipindi wanawake hupata sana UTI

UTI sio ugonjwa wa kawaida au mdogo tu kama watu wengi wanavyodhani , unajua kwanini ? Ni kwasababu UTI huweza kuharibu kabisa FIGO zako na hata kuharibu pia mirija inayotoa mkojo kwenye figo kwenda kwenye kibofu (ureters) , lakini UTI yaweza pia kuathiri sana kibofu chako cha mkojo , kwahiyo sio ugonjwa wa kuuchukulia poa


TUANGALIE NINI KISABABISHI CHA UTI KIPINDI CHA UJAUZITO ?

  • Utapata UTI kwa sababu ya bacteria ( E.coli na Chlamydia) ambao wapo zaidi katika ngozi yako , puru au katika uke
  • Kubadilika kwa muundo wa mfumo mzima wa mkojo , kuanzia kwenye figo , ureters kubanwa na hata kibofu kusukumwa na kuwa na nafasi ndogo
  • Kibofu kutotoa mkojo wote na hivyo mkojo unaobaki unakua ulio mkali (concentrated) wenye sukari, hormones na proteins na asidi
KWANINI UTI INAWAPATA SANA WAJAWAZITO ?

Sababu kuu hasa ni kwasababu mtoto anavyokua akiwa tumboni hukandamiza kibofu , na kupelekea hali ya mjamzito kutomaliza mkojo anapokojoa , yani hakojoi mkojo wote ukaisha , sasa hii hupelekea hali ya bacteria kukua kwa kasi

Hormones pia huweza pelekea mabadiliko kadhaa katika mfumo wa mkojo , jambo ambalo pia huweza changia bacteria kukua kwa urahisi zaidi


TUONE DALILI ZA UTI KWA MJAMZITO.....

Sio wakati wote unapokua na UTI utajua hapana . Asympomatic UTI unapokua nayo hutosikia dalili zozote ila daktari anaweza gundua baada ya vipimo na akakushauri chakufanya

Lakini kwa Smptomatic UTI (UTI inayoonesha dalili ) basi utakutana na dalili kama hizi :
  • Hali ya kuchoma na maumivu unapokojoa
  • Maumivu sehemu ya kibofu kilipo
  • Mkojo waweza kuwa na damu
  • Mkojo unaweza onekana wenye rangi mawingu /ukungu hivi
  • Unaweza pia ukapata maumivu na usifurahie tendo la ndoa
  • Kujisikia kukojoa mara kwa mara
  • Homa na kutokwa jasho
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya kiuno

TIBA IKOJE KWA WAJAWAZITO ?

Tiba itahusisha dawa aina ya antibiotics , ambazo zitatumika kwa muda wa siku 3 hadi 7 kadiri daktari atakavyokushauri . FDA imependekeza zaidi antibiotics kama vile erythromycin, amoxicillin, and penicillin kuwa salama zaidi kwa mjamzito (Category A) katika kutibu UTI , Dawa zingine ni kama vile Nitrofurantoin n.k
Dawa zote hizo hazishauriwi kutumika bila ushauri au maelekezo ya Mfamasia au Daktari

HAYA NI BAADHI YA MAMBO UNAYOWEZA KUYAFANYA NYUMBANI KUPUNGUZA UKUBWA WA TATIZO HILI LA UTI
  • Kunywa maji mengi , husaidia kuondoa bacteria kadiri unavyokojoa
  • Vitunguu swaumu (Waweza tumia punje 3 hivi , asubui na jioni)
  • Maji ya nazi /dafu au maziwa ya nazi , husaidia pia
  • Tumia vitamin C kwa wingi , waweza ipata kwenye matunda kama machungwa , berries, nyanya kwa wingi. Huongeza kinga ya mwili hivyo inarahisisha uwezo wa mwili kupambana na bacteria
  • Apple cider vinegar
UNAJIKINGA VIPI NA UTI UNAPOKUA MJAMZITO ?

Japo hakuna uhakika wa asilimia 100 kwamba utajikinga moja kwa moja , ila kuna baadhi ya mambo ukizingatia basi yatakupa uhakika kidogo wa kutopata hili gonjwa mara kwa mara

  • Usikae na mkojo mda mrefu , ukijisikia tu kukojoa nenda kamalize shuguli
  • Nawa kutoka mbele kwenda nyuma , kuepusha bacteria kuingia katika tundu la mkojo , nshauri zaidi ujifute kwanza kwa Toilet paper (Paper towel) kabla hujanawa
  • Osha sehemu zako za siri (nje) kwa kutumia sabuni isiyokua na kemikali au manukato sana , na maji , na uwe mkavu mda mwingi
  • Safisha sehemu zako za siri kabla na baada ya ngono (sex)... Nadhani tunaelewana naposema safisha sehemu za siri (Nilishafundisha namna unayopaswa kujisafisha )
  • Wale mnaotumia bathtub  , usikae humo kwa zaidi ya nusu saa , wala zaidi ya mara mbili kwa siku
  • Epuka vipodozi vikali , wala usijipake au kujipulizia maeneo yako ya siri , maana itachangia kukupa miwasho, michubuko na hata bacteria kuzaliana
  • Punguza matumizi ya vyakula vya viwandani na sukari kwa wingi , maana hupelekea ukuaji wa bacteria kuwa mrahisi
  • Epuka kuvaa nguo zinazobana sana , vaa nguo za ndani ambazo zimetengenezwa kwa pamba na zisikubane

JE, UTI INAWEZA KULETA MADHARA KWA UJAUZITO ?

Ndio , endapo UTI itakurudia mara kwa mara au ikadumu kwa muda mrefu , italeta shida na huenda usipate ujauzito kirahisi , kwasababu figo , mfuko wa uzazi na mirija ya uzazi (Fallopian tubes) huweza kuathiriwa na ugonjwa huu

NADHANI KILA ALIYESOMA AMENIELEWA VIZURI HIVYO BASI SIO VIBAYA UKIMWELEKEZA MJAMZITO KUHUSU HAYA MAMBO YA MSINGI NILIYOYAFUNDISHA HUWEZI JUA UTAMSAIDIA KWA KIWANGO GANI , HUENDA NI TATIZO LINALOMSUMBUA SANA  

No comments:

Post a Comment